"Weltwärts" kutoka kusini kwenda kaskazini
kutoka kwa Nancy Towo
Moja ya mambo ambayo RAFIKI imeweza kufanya ni pamoja na kuweza kuleta vijana wa kujitolea kutoka Tanzania. Kwa majina ni Mercy Lymo na Nancy Towo , sisi tumeweza kuwa wa kwanza kwenye mafanikio haya kuweza kukaa kwa miezi tisa nchini ujerumani. Tulifika mwezi wa desemba mwaka jana. Ilikuwa baridi sana ambayo hatujawahi kuihisi. Kiongozi wetu alikuwepo na kila tulipokuwa na shida alitusaidia. Hii imeweza kuwa fursa nzuri kuweza kuona tamaduni tofauti na maisha mengine zaidi ya tuliyozoea
Malazi
Tulifika nyumba kwetu ambayo ni mabweni ya BiBeKu ambapo kila mmoja wetu alipatiwa chumba chake. Tunapaita pa kimataifa kwa sababu tunakaa na vijana wa Ujerumani na kutoka maeneo mengine pia. Kwa mchana tunakula chakula kizuri kila siku kutoka kwa BiBeKu . Na kwa asubuhi na jioni tunaandaa wenyewe kama tutakavyo penda. Kwa siku nyingine tunapika pamoja na wenzetu mapishi tofauti
Mazingira
Kellinghusen ni kijiji kilichopo kwenye eneo la Schleswig-Holstein. Kijiji hichi kina mazingira mazuri sana. Watu pia wanaoishi hapo ni wakarimu sana. Tunaishi karibu sana na msitu na ziwa dogo ambavyo vinafanya mazingira yaendelee kuwa mazuri. Zaidi ya hayo pia kuna mto umepita kwenye kijiji hichi.
Kazi
Kazi ambazo tunafanya ni kutokana na kitu tunachopenda. Mimi ninafanya kazi kwenye kutafsiri tovuti ya RAFIKI kutoka kingereza kwenda Kiswahili. Na mwenzangu anafanya kazi kwenye chekechea ambayo ipo Kellinghusen. Tunafanya miradi mingine pamoja kama kupika chakula cha kitanzania kwenye sehemu mbalimbali kama kwenye nyumba ya jamii iliyopo kellinghusen. Pale kunapokuwa na vikao vya RAFIKI tunapenda pia kuandaa vyakula vya kitanzania. Pia tunatoa mafunzo ya Kiswahili kwenye chuo kikuu cha Christian albert. Zaidi ya hayo tunatembelea shule ambazo zina klabu za kiafrika na kuwaeleza kitu kuhusu Tanzania.
Kujua lugha
Tulitakiwa kuanza kujifunza lugha. Tulitafutiwa mwalimu mzuri sana anayeitwa Janna kutoka Kellinghusen. Kipindi chetu cha kusoma kijerumani kilikuwa kila siku kwa lisaa limoja kwanzia siku za kwanza. Kwangu haikuwa ngumu sana kwa kuwa nilishasikia hii lugha kabla ya kuja Ujerumani ila kwa Mercy ilikuwa ngumu kwa kuwa ilikuwa mara yake ya kwanza. Ila licha ya hayo tulifurahia kujifunza lugha pamoja.
Zaidi ya kufanya kazi kwa RAFIKI tunaweza kufanya mambo mengine pia.Tumepata nafasi ya kujiunga na timu ya volleyball iliyopo Wrist kijiji kilichopo karibu na Kellinghusen. Pia tumeweza kuwa tunaangalia michuano ya mpira wa miguu wa wanawake. Tumeweza kutembelea maeneo mbalimbali ya ujerumani kama Hamburg. Pia tulifanya safari pamoja na kiongozi wetu(Marcus Wack) na rafiki yetu (Simon Dickmann) kwenda Berlin. Tulizunguka kwenda maeneo mbalimbali ya mji wa Berlin na kujifunza kuhusu kupunguza matumizi ya plastiki na pia kukusanya mawazo ya jinsi mbalimbali ya kuweza kutumia tena matakataka.